Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Kampuni za usafirishaji kuwabaini wasafirishaji dawa za kulevya

Imewekwa: 02 November, 2021
Kampuni za usafirishaji kuwabaini wasafirishaji dawa za kulevya

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya (DCEA) Gerald Kusaya ameambatana na Makamishna wengine wa Mamlaka kulitembelea Shirika la Posta Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na kujionea namna ambavyo Shirika hilo linadhibiti usafirishaji wa dawa za kulevya.

Katika ziara hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam, Kamishna jenerali Kusaya amewataka wasafirishaji wa mizigo kupitia Kampuni mbalimbali Nchini, kuwa wazalendo na waaminifu kwa kutojiingiza katika shughuli za dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kukagua kwa makini mizigo wanayoisafirisha ili kuepukana na udanganyifu unaoweza kufanywa na wateja wao.

"Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya tunahakikisha tunapambana na wanaoshughulika na uuzaji na usambazaji wa dawa hizi, na kuhakikisha hakuna dawa inayoingia Nchini na ndio maana tumekuja hapa kuangalia mifumo ya usafirishaji wa mizigo ya Posta, nimejionea na kwa kweli wanadhibiti hali hiyo, wana mashine za kisasa" amesema Kamishna Kusaya.


dKamishna Jenerali Kusaya akifafanua jambo kwa uongozi wa Shirika la Posta wakati wa ziara yake jijini Dar es Salaam.

Nae Kaimu Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo amesema Shirika la Posta limejipanga katika kuhakikisha hakuna dawa ya kulevya inayosafirishwa kupitia Shirika hilo.

"Naomba niwaambie wanaodhani hapa Posta ni mlango wa kupitishia dawa za kulevya, hapa sio mahali pake, tupo makini sana, tuna vifaa vya kisasa, tuna wataalamu wa kutosha,na ukijaribu tutakubaini haraka sana, pia tunashirikiana na mashirika ya Posta Duniani kudhibiti usafirishaji wa dawa hizi" amesema Bw. Mbodo.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekuwa ikishirikiana kwa ukaribu na Shirika la Posta Tanzania kwa nia ya kuongeza kasi ya udhibiti wa uingizaji na usambazaji wa dawa za kulevya Nchini.


MWISHO