Kamati ya Bunge Zanzibar Yafanya Ziara DCEA, Yajifunza Uchunguzi na Sayansi Jinai

Kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogondogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imefanya ziara katika ofisi za makao makuu Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania Bara. Lengo kuu la ziara hii ni kujifunza shughuli zinazotekelezwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika eneo la sayansi jinai na kubadilishana uzoefu kuhusu teknolojia za kisasa zinazotumiwa katika uchunguzi wa dawa za kulevya.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati wamepata nafasi ya kutembelea maabara ya DCEA na kuona vifaa mbalimbali vinavyotumika katika maabara hiyo, kupata taarifa kuhusu tafiti zilizofanywa na zinazofanyika kuhusu vitu mbalimbali vinavyotumika kama dawa za kulevya pamoja na kushuhudia namna ya ufanyaji wa uchunguzi awali katika utambuzi wa dawa za kulevya.
Kaimu kamishna wa Ukaguzi na Sayansi Jinai wa Mamlaka Bw. Ziliwa Machibya amewaeleza wajumbe kuwa, katika muktadha wa dawa za kulevya, Sayansi jinai ni matumizi ya sayansi kutoa majibu ya kitaalamu katika utambuzi wa dawa ili taratibu za kisheria ziweze kuendelea ikiwa ni hatua muhimu kabla ya kutekeleza zoezi la operesheni ili kuweka uhakika kwamba kinachotakiwa kukamatwa ni dawa za kulevya.
Aidha, wajumbe wamepata nafasi ya kusikiliza mada, kuuliza masuala mbalimbali ya kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mamlaka Tanzania Bara, na kupata majibu kutoka kwa wataalamu wa maeneo yao ili kupata uelewa wa pamoja.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Mihayo Juma Nhunga amesema kama kamati wamevutiwa na maendeleo makubwa yanayofanywa na DCEA katika udhibiti wa dawa za kulevya Tanzania bara, hivyo wameona ni vema kutumia nafasi hii kujifunza masuala ya uchunguzi na sayansi jinai ili waweze kuboresha katika maeneo yao.
Nae Kamishna jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar Kanal Burhani Zubeir Nassoro Zahoro ameishukuru Mamlaka Tanzania bara kuwapokea na kuwaruhusu kujifunza.
“Nilikuwa naulizwa hili suala, ni kwanini tuwe na maabara wakati ofisi ya mkemia ipo? Lakini sasa tumepata majibu maabara hii ni muhimu kumsaidia mpelelezi kukamilisha uchunguzi wake ili kielelezo kipelekwe kwa mkemia” amesema.
Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kusisitiza umuhimu wa Taasisi zote za Jamhuri ya Muungano kushirikiana kwani ushirikiano huu unaleta manufaa sana.
“Sisi tunajiandaa kuanzisha hiyo maabara, lakini tunajua ni gharama hivyo tunaiomba Kamati ya Bajeti mtusaidie tunapoleta bajeti yetu ili tuweze kuanzisha maabara hii ya sayansi jinai” amesisitiza Kanal Nassoro.
Naye, Mwanaasha Khamis Juma, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti anaemwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la wawakilishi Zanzibar amesema;
“Kamati yetu imekuja kwa nia ya kujifunza kweli kweli na tumepata tulichokihitaji ili kujua nini tutafanya katika kudhibiti dawa za kulevya. Haya tunayafanikisha kutokana na pande zote kuwa na dira na dhamira moja katika kupambana na dawa za kulevya”
Ameongeza kuwa, changamoto ya uwepo wa dawa mpya za kulevya iko pande zote mbili yaani Bara na visiwani kwa hili naomba Mamlaka zote zikae pamoja kuona ikiwa kuna uwezekano wa kuliweka katika sheria ili kuweza kudhibiti vizuri.
“Sisi kama kamati tulihisi uwepo wa maabara utaleta mwingiliano kati ya ZDCEA na Mkemia Mkuu wa Serikali kumbe sivyo, hivyo tumekuja kama kamati, Mamlaka na watu wa mkemia mkuu wa serikali na kwa upande wetu tumejifunza na tutazipitia vizuri kanuni zetu kuona namna ya kulitekeleza hili. Maeneo yenye mashaka tutayaweka vizuri na kazi itaendelea.” amesisitiza Mwanaasha Juma.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania Bara Aretas Lyimo amewashukuru wajumbe kwa kuamua kuchagua kujifunza Tanzania na sio nchi yoyote kwani adui wanaepigana nae ni mmoja hivyo kuunganisha silaha ni mbinu ya kumshinda adui huyo.
Sambamba na hilo amesisitiza suala la uelimishaji lipewe kipaumbele kwani watu wakielimika watatoa ushirikiano dhidi ya wahalifu wa dawa za kulevya.
Ziara hii inachukuliwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano kati ya udhibiti wa dawa za kulevya Tanzania Bara na Visiwani huku ikilenga kuboresha mbinu za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.
Mkemia kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Bi. Sarah Lija akiwaonesha matokeo ya upimaji wa sampuli za dawa za kulevya katika maabara ya DCEA kama hatua muhimu za kioperesheni.
Kamishna msaidizi wa Ukaguzi na Sayansi Jinai DCEA Bw. Ziliwa Machibya akifafanua jambo kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogondogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar walipotembelea maabvara ya DCEA
Baadhi ya wajumbe wakichangia mada kwenye kikao kilicholenga kujifunza shughuli zinazotekelezwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika eneo la sayansi jinai
Kamishna wa Huduma za Sheria DCEA Bi. Veronica Matikila akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali ya kisheria
Kamishna msaidizi wa Ukaguzi na Sayansi Jinai Ziliwa Machibya akiwasilisha mada
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti anaemwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Sheria Ndogo ya Baraza la wawakilishi Zanzibar Mhe. Mwanaasha Juma akitoa neno la shukrani kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati.
Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogondogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wakizungumza na Kamishna Jenerali DCEA mara baada ya kuwasili ofisi za DCEA makao makuu.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogondogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mihayo katika picha ya pamoja na makamishna jenerali wa DCEA na ZDCEA pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati.
Kamishna msaidizi wa Ukaguzi na Sayansi Jinai DCEA Bw. Ziliwa Machibya akitoa maelezo ya awali kuhusu maabara kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogondogo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Picha ya pamoja ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya sheria ndogondogo ya Baraza la Wawakilishi pamoja na viongozi wa DCEA na ZDCEA
Mwisho