Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

Wanahabari ni wadau muhimu katika mapambano ya dawa za kulevya

Imewekwa: 16 January, 2026
Wanahabari ni wadau muhimu katika mapambano ya dawa za kulevya

 

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya kikao kazi maalum kilichowakutanisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja, kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati madhubuti ya utoaji wa taarifa na elimu kwa jamii kuhusu mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Kikao kazi hicho kilifanyika Ijumaa, tarehe 9 Januari 2026, katika ukumbi wa Four Points by Sheraton Posta, Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na waandishi wa habari pamoja na wataalamu kutoka DCEA.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alisema kuwa tatizo la dawa za kulevya linaathiri kwa kiasi kikubwa afya, usalama na maendeleo ya jamii. Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya tatizo hilo hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya Mamlaka na vyombo vya habari.

Alieleza kuwa DCEA imeendelea kushirikiana na vyombo vya habari kupitia utoaji wa taarifa rasmi, mikutano na waandishi wa habari, mahojiano pamoja na programu mbalimbali za uelimishaji wa jamii, hatua ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

“Mchango wa waandishi wa habari ni muhimu na haukwepeki. Taarifa zinazotolewa na vyombo vya habari zimekuwa chachu ya mafanikio katika kufichua mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya, kuhamasisha waraibu kujiunga na huduma za tiba, kuondoa sintofahamu katika jamii, pamoja na kuchochea mabadiliko chanya ya tabia, hususan kwa vijana,” alisisitiza Kamishna Jenerali.

Katika majadiliano, waandishi wa habari walibainisha kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuibua na kuonesha athari za matumizi ya dawa za kulevya kwa jamii kupitia taarifa na vipindi vya elimu. Hata hivyo, changamoto za kiuchumi na kifedha zimeathiri uendelevu wa baadhi ya vipindi maalum vya elimu, hali inayopunguza wigo wa kufikia jamii kwa ufanisi.

Aidha, ilielezwa kuwa bado kuna changamoto katika kudhibiti vyanzo na njia za uingizaji wa dawa za kulevya kutoka nje ya nchi, jambo lililoonesha umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kikanda pamoja na uandishi wa habari wa kuvuka mipaka (cross-border journalism).

Kutokana na mjadala huo, kikao kazi kiliweka msisitizo katika matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo majukwaa ya kidijitali, wahamasishaji wa mitandaoni na mbinu bunifu za mawasiliano, ili kuongeza ufanisi wa elimu kwa jamii. Vilevile, ilisisitizwa haja ya kujenga uwezo wa waandishi wa habari katika kuandaa maudhui yenye mvuto, uzito na athari chanya katika kupambana na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Kikao kazi hicho kimeweka msingi imara wa kuimarisha ushirikiano kati ya DCEA na vyombo vya habari, na DCEA imeahidi  kuendelea kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili waweze kuripoti masuala ya dawa za kulevya kwa usahihi, weledi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya umma.