Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Hekari101 na Magunia 482 ya bangi yateketezwa Arusha

Imewekwa: 01 June, 2023
Hekari101 na Magunia 482 ya bangi yateketezwa Arusha

Kufuatia agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kufanya operesheni ili kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa Nchini, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama jana tarehe 31 Mei, 2023 imeteketeza zaidi ya hekari 101 za mashamba pamoja na magunia 482 ya dawa za kulevya aina ya bangi katika eneo la Kisimiri juu kata ya Uwalu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Akiongoza operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha bangi inatokomea kabisa na wananchi wanajikita katika mazao mengine ya biashara badala ya bangi.

Kamishna Lyimo amesema, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) katika kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais linatekelezwa, ameelekeza kufanyika kwa utafiti kujua ni mazao gani mbadala yanaweza kulimwa katika maeneo hayo ambayo yamekithiri kwa kilimo cha dawa za kulevya, ili wananchi wa maeneo husika waweze kupewa mbinu mbadala za kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara badala ya kuendelea na kilimo cha bangi.

‘‘Tumewasiliana na Wizara ya Kilimo na Afisa kilimo wa kata ya Uwalu hapa Kisimiri ambaye ameeleza tayari utafiti huo umefanyika",amesema.

Aidha, Kamishna Lyimo amesema, elimu juu ya athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya itatolewa kupitia shule za msingi na sekondari.

"Hii inafanyika kufuatia agizo la Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kuitaka Mamlaka kushirikiana na wadau kutoa elimu katika maeno hayo. ambapo tayari maafisa elimu Kata wameanza kutoa elimu kwa wanafunzi, ili baadaye wasijihusishe na

Operesheni hii mkoani Arusha imefanyika ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mheshimiwa Jenista Mhagama (Mb) kutoa taarifa ya hali ya dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022 ambapo katika taarifa hiyo alitaja mikoa inayojihusisha na kilimo cha Bangi kwa kiasi kikubwa huku mkoa wa Arusha ukiwa kinara ukifuatiwa na Iringa, Morogoro na Manyara.