Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Hekari 10 za mirungi zaharibiwa mkoani Kilimanjaro

Imewekwa: 20 December, 2021
Hekari 10 za mirungi zaharibiwa mkoani Kilimanjaro

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi imeharibu zaidi ya hekari 10 za mashamba ya dawa za kulevya aina ya mirungi katika kitongoji cha Kindi, kijiji cha Likweni, kata ya Tae, wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

Aidha, katika zoezi hilo watu wawili wanashikiliwa kwa tuhuma za kusafirisha zaidi ya bunda 270 ya dawa za kulevya aina ya mirungi.

Akizungumzia operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya amesema Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama na Mamlaka nyingine za udhibiti, imejipanga katika kudhibiti biashara hiyo lengo likiwa ni kumaliza kabisa tatizo la dawa hizo.

“Tunataka kuwa na Tanzania isiyokuwa na watu wanaojihusisha na dawa za kulevya, tunashirikiana vema na Mamlaka nyingine za udhibiti, lengo letu ni kuhakikisha kuwa tunamaliza kabisa tatizo hilo Nchini, ili mwisho wa siku tuwe na Tanzania isiyokuwa na dawa za kulevya na hii inawezekana. Niwaombe watanzania wenye mapenzi mema na nchi yao kutoa taarifa za watu wanaojiuhusisha na biashara hii” amesema Kamishna Jenerali Kusaya.Hekari 10 za mirungi zaharibiwa mkoani Kilimanjaro

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro ACP. Simon Marwa Maigwa amesema katika kipindi cha kuanzia Mwezi Januari mpaka Septemba mwaka 2020, jumla ya kesi 540 za dawa za kulevya zilizowahusisha watuhumiwa 467ziliripotiwa mkoani humo. Vilevile katika kipindi hicho hicho kwa mwaka 2021 jumla ya kesi 678 ziliripotiwa zikiwahusuisha watuhumiwa 561 ambapo kesi hizo zipo katika hatua mbalimbali mahakamani.


MWISHO