Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA yatoa vifaa tiba kwenye vituo vidogo vya kutolea huduma ya Methadone jijinii Dar Es Salaam

Imewekwa: 21 November, 2021
DCEA yatoa vifaa tiba kwenye vituo vidogo vya kutolea huduma ya Methadone jijinii Dar Es Salaam

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imekabidhi vifaa tiba pamoja na samani mbalimbali katika vituo vidogo (satelite clinics) vya kutolea tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya. Vituo hivi viko katika Hospitali ya Vijibweni wilaya ya Kigamboni, Mbagala round Table Wilaya ya Temeke, Tegeta Wilaya ya Kinondoni pamoja na zahanati ya gereza la Segerea katika Wilaya ya Ilala.

Hatua hii ni katika kutekeleza mkakati wa kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya ambao ni moja ya mkakati unaotumiwqa na Mamlaka kutekeleza majukumu yake ambapo Mamlaka inajukumu la kusimamia uanzishwaji na uendeshwaji wa vituo vya kutolea tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya nchini (MAT Clinics).

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo katika kituo kilicho zahanati ya gereza la segerea Kamishna Jenerali Gerald Kusaya amesema hadi sasa kuna vituo 11 vya methadone Nchini ambapo vyote kwa pamoja vimesajiri waraibu wapatao 10,600. Vituo hivi viko katika mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Dodoma, Arusha, Tanga, Pwani na Songwe.


Katika mkoa wa Dar es Salaam kuna vituo vitatu ambavyo kila kimoja kinahudumia kati ya waraibu 1,100 hadi 1,300 kwa siku. Kutokana na wingi wa waraibu wanaopatiwa tiba katika vituo vilivyopo katika mkoa wa Dar es Salaam, Serikali kwa Kushirikiana na Wadau wa Maendeleo (Global Fund) iliamua kujenga vituo vingine vidogo vinne (satellite clinics) vya kutolea methadone katika mkoa wa Dar es Salaam ili kupunguza msongamano katika vituo..

Aidha, kamishna Kusaya amesema kwamba, Mamlaka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na wadau wengine imetoa mafunzo kwa watoa huduma wa afya watakaokuwa wanafanya kazi katika vituo husika.

"Kituo hiki cha Segerea kitatoa huduma kwa mahabusu na wafungwa wanaohitaji huduma hii pamoja na waraibu wengine wanaozunguka eneo hili. pia uwepo wa vituo hivi utapunguza msongamano katika vituo vya Dar es Salaam na kurahisisha kuwafikia wahitaji walioko katika maeneo ya mbali. Hivyo uwepo wa vituo hivi utapunguza gharama kwa wahitaji na kupunguza mzigo kwa wahudumu wa afya" amesema Kamisha Jenerali Kusaya.

Ameongeza kuwa Mamlaka kwa kushirikiana na wadauu wengine itahakikisha inaongeza vituo hivi katika kila mkoa Nchini.

Kwa upande wake kamishna msaidizi wa Magereza Dar es Salaam, ACP Focus Ntakandi ameishukuru Manala kwa kupekela vifaa hivyo kituoni hapo ili kuwasaidia wafungwa ambao wameathirika na dawa za kulevya. na kuiomba Mamlak kuongeza vituo vingine katika magereza mbalimbali.


Mwisho