Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA Yatoa Jumla ya Lita 261,750 za Kemikali aina ya Ethyl Alcohol ili Zitumike Kutengeneza Vitakasa Mikono

Imewekwa: 21 April, 2020
DCEA Yatoa Jumla ya Lita 261,750 za Kemikali aina ya Ethyl Alcohol  ili Zitumike  Kutengeneza Vitakasa Mikono

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imetoa jumla ya lita 261,750 za kemikali aina ya Ethyl Alcohol kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ili zitumike katika kutengeneza vitakasa mikono (hand sanitizers) na kukabilina na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (covid 19).

Makabidhiano hayo yamefanywa na Kaimu Kamishna Jenerali wa Mamlaka James Kaji ambapo Lita 170,000 zimekabidhiwa mbele ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda na lita 91,750 zimekabidhiwa kwa mkuu wa mkoa wa Mwanza.

Wakati wa makabidhiano hayo kamishna Kaji amesema kemikali hizo zimetolewa kutokana na agizo la serikali ili zitumike kutengenezea vitakasa mikono na kusaidia kupunguza gharama za bidhaa hiyo kwa wananchi. ‘‘kutokana na hali ya ugonjwa tuliyonayo hasa kwa mkoa wa Dar es Salaam tuliona ni jambo jema kuwasiliana na uongozi wa mkoa ili kuunga mkono jitihada za mkoa katika kupambana na ugonjwa wa corona kwa kutoa hizi kemikali ambazo zitasaidia katika kutengeneza vitakasa mikono’’ amesema kamishna Kaji.J

Naye mkemia mkuu wa serikali Fidelis Mafumiko amesema baada ya kukabidhiwa kemikali hizo walichukua sampuli na kuiangalia ubora wake ambapo wamejiridhisha kwamba kemikali iliyotolewa inakidhi viwango vya ubora katika kutengeneza vitakasa mikono.

RC Makonda ameipongeza Mamlaka kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kupigania na kuokoa maisha ya watanzania. Pia amezishukuru Mamlaka zote zilizohusika katika kufanikisha ukamataji na uhifadhi wa kemikali hizo.

Aidha amesema kemikali hizo zitatolewa kwenye viwanda vyote vinavyotengeneza vitakasa mikono vilivyosajiliwa na serikali na vyenye utaratibu wa kuuza bidhaa zao kwa Bohari kuu ya Dawa (MSD) ambapo amesema atavielekeza vyombo vya ulinzi kupita na Kudhibiti kupanda kwa bei ya bidhaa hizo ili kila mwananchi bila kujali hali ya kipato chake aweze kumudu gharama za bidhaa hiyo.

Kemikali zilizotolewa zilikamatwa kutokana na kuingizwa nchini kinyume cha Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani namba 3 ya mwaka 2003, hivyo zilizuiliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya udhibiti wa kemikali. Kufuatia kukamilika kwa hukumu ya mahakama kemikali hizo zilitaifishwa na kuwa mali ya serikali.