Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA yashiriki Maonesho Wiki ya Sheria

Imewekwa: 25 January, 2023
DCEA yashiriki Maonesho Wiki ya Sheria

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Musabila Kusaya amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Disemba 2021 mpaka sasa jumla ya watumiaji 12,800 wa dawa za kulevya wameamua kuachana na matumizi hayo na kukubali kwenda katika vituo vya Methadone kwa ajili ya kutibiwa.

Kamishina Jenerali Kusaya amesema hayo katika maonyesho ya wiki ya sheria yanayofanyika jijini Dodoma Katika viwanja vya Nyerere (Nyerere Square) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa idadi ya waathirika waliojitokeza kupata tiba ni matokeo ya kazi kubwa inayofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya hasa katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya tatizo la dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na Kudhibiti matumizi na Kupambana na biashara ya dawa hizo.

“Mamlaka imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusiana na Sheria za dawa za kulevya pamoja na madhara yatokanayo na dawa hizo. Matumizi na biashara ya dawa za kulevya yamepungua kwa kiasi kikubwa, wengi wameacha na wengine wameamua kujisalimisha ili kupata matibabu katika vituo vya serikali” amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Akiendelea kubainisha hayo, amesema Tanzania imefanya vizuri zaidi kwa nchi za Afrika Mashariki katika eneo la kutoa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya ambapo mpaka sasa kuna vituo vya Methadone 15 nchi nzima.

Aidha, amebainisha kuwa kutokana na uimara katika udhibiti wa dawa za kulevya, watumiaji wa dawa za hizo wamebuni mbinu mpya na kuanza kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya kama mbadala wa dawa za kulevya.

“Matumizi ya heroin, bangi na mirungi yamepungua kwa kiasi kikubwa, sasa hivi wameanza kutumia dawa tiba za binadamu kama vile Valium, Tramadol, Ketamine na nyinginezo, kama mbadala lakini wapo pia wanaotumia rangi, na petroli na gundi" amesema Jenerali Kusaya.

Pia, amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itaendelea kudhibiti uingizwaji kemikali bashirifu ambazo zikichepushwa zinaweza kutumika kutengeneza dawa za kulevya pamoja na kuimarisha ushirikiano na vyombo vingine vikiwemo Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) ili kuona namna ya kufanya kuhusu matumizi ya shisha, rangi na petrol.

Pamoja na hayo, Kamishna jenerali Kusaya amesema kuwa kwa kipindi cha Disemba 2021, mpaka Disemba 2022 Mamlaka imefanikiwa kuzuia uingizwaji wa kilo 120 na lita 85 za kemikali bashirifu.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya ni moja ya wadau wanaoshiriki katika Maonesho ya Wki ya Sheria jijini Dodoma, iliyofunguliwa tarehe 22 mwezi Januari, 2023 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 29 ya mwezi huu.