Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA yang'ara tuzo za uandaaji wa taarifaza za fedha viwango vya kimataifa

Imewekwa: 06 December, 2021
DCEA yang'ara tuzo za uandaaji  wa taarifaza za fedha viwango vya kimataifa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekuwa mshindi na kupata tuzo mbili katika hafla ya ugawaji tuzo hizo iliyoandaliwa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania ( NBAA) na kufanyika siku ya Ijumaa tarehe 03 Desemba 2021 katika ukumbi wa APC ulioko Bunju jijini Dar es Salaam.

Tuzo ya kwanza ni tuzo ya umahiri katika uandaaji wa taarifa za fedha ya mwaka 2020 kwa viwango vya kimataifa kwa sekta za umma (IPSA) katika kundi la Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea (MDAs), na tuzo ya pili ni ya mshindi wa jumla wa kundi hilo.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa washindi na kupata tuzo, kamishna jenerali Gerald Kusaya amesema pamoja na kazi ya kupambana na dawa za kulevya pia Mamlaka huweka jitihada katika kuangalia jinsi ambavyo rasilimali fedha zinatumika kama ilivyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuweka vizuri kumbukumbu za mahesabu.

Pia, Kamishna Jenerali Kusaya amesema siri ya ushindi ni umoja na mshikamano ndani ya Mamlaka kuanzia kwake yeye kama Mtendaji Mkuu, kwa wasaidizi wake; hivyo anapotoa maelekezo yanasikilizwa na kutekelezwa vizuri zaidi na wale walioko chini yake kwa maana ya wahasibu na watu wote wanaohusika kutunza kumbukumbu ndani ya mamlaka na ndio maana Mamlaka inaendelea kufanya vizuri.

"Unapokuwa na matumizi mazuri ya kifedha ndio yanayosababisha taasisi kuwa na hesabu nzuri za kifedha, kwa watendaji wakuu tunachotakiwa kufanya kwanza kuifahamu taasisi unayoiongoza na kisha kutoa maelekezo na kuyafauatilia kwa karibu kuona kama yanafanyiwa kazi. Lazima tuzingatie sheria na miongozo ya umma. Malengo ya mamlaka hii ni kuendelea kuibuka na ushindi. amesema Kusaya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya imeendelea kupata ushindi na kupokea tuzo mara mara nne mfululizo tangu mwaka 2017.


h