Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA yafanya ziara uwanja wa ndege wa Julius Nyerere

Imewekwa: 23 July, 2023
DCEA yafanya ziara uwanja wa ndege wa Julius Nyerere

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo akiambatana na viongozi wengine wa Mamlaka, amefanya ziara ya kikazi katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kufanya kikao na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya uwanja huo kwa lengo la kujadili na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji utakaosaidia kudhibiti usafirishaji na uingizaji wa dawa za kulevya nchini kupitia uwanja huo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho kamishna Lyimo amesema lengo kuu la ziara hiyo ni kujitambulisha kwani anatambua JNIA ni wadau muhimu wa Mamlaka na wanashirikiana katika kazi. Pia, ziara hiyo ni muhimu katika kuimarisha ushirikano kati ya Mamlaka na viwanja wa ndege ili kupambana na dawa za kulevya kwani baadhi ya waharifu wa dawa za kulevya wanatumia viwanja vya ndege kuingiza na kutoa dawa hizo.


“Viwanja vya ndege ni vituo muhimu sana katika udhibiti wa dawa za kulevya kwa kuwa duniani kote viwanja vya ndege hupitisha dawa za kulevya. kwahiyo tukiimarisha mahusiano na kushirikiana tunaweza kulimaliza hili tatizo. Amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Aidha, amewaomba watumishi wa uwanja wa ndege kushiriki katika mapambano kwa kutoa taarifa za watu wanaosafirisha dawa hizo ikiwa ni pamoja na kutoa ushahidi mahakamani pale inapohitajika.

“Kuna kesi ambazo tunazianzisha zikitokea airport, sasa kuna wale maafisa wa airport ambao huwa wanashuhudia tunaomba wasiwe na wasiwasi kwenda mahakamani kutoa ushahidi, pia wawe wanatoa taarifa kwetu pale wanapowabaini waharifu wa dawa za kulevya. Mtoa taarifa awe na uhakika kwamba taarifa yake italindwa na hakuna mtu atakayemjua kwamba ni yeye aliyetoa taarifa” amesema kamishna Jenerali Lyimo.

Nae Kamishna wa Kinga na Tiba Dkt. Peter Mfisi amesema ni muhimu kujua nchi inatumia rasilimali nyingi kupambana na dawa za kulevya kutokana na madhara yanayotokana na matumizi na biashara ya dawa hizo.

Hivyo, ameomba kupata nafasi ya kutoa elimu mara kwa mara kwa watumishi wa uwanja wa ndege kuwaeleza jinsi ya kugundua dawa za kulevya, Pamoja na madhara dawa hizo katika nyanja zote za maisha ili waweze kuelewa umuhimu wa kupambana na dawa za kulevya na kuchukua hatua pale wanapowabaini wanaosafirisha dawa za kulevya.

“Nchi yetu ni kama transit country, dawa zinaingia na kutoka, lakini zinapotoka kuna nyingine nyingi zinabaki kwahiyo unapomuona mtu anasafirisha dawa za kulevya Kwenda nje ujue na hapa nchini anauza. Hivyo, ukimkamata utamfanya asizisafirishe kule anakozipeleka na asiziuze huku kwa watu wetu” amesema Dkt. Mfisi.

Kwa upande wa mkurugenzi wa JNIA Bi. Rehema Myeya amesema wako tayari na wanahitaji sana kupata mafunzo kutoka DCEA kwa ajili ya kuwasaidia maafisa wao kupata uelewa kuhusu dawa za kulevya. Pia amesisitiza umuhimu wa kubadirishana taarifa kati ya DCEA na JNIA ili kufanikisha azma njema ya kupambana na uhalifu.

Ameongeza kuwa unyeti wa suala la dawa za kulevya linahitaji watu wote kuwa wazaendo kwani nchi yoyote inafanikiwa kutokana na uzalendo.

“Wakati mwingine mtu anapanda ndege akiwa free anaenda kumeza dawa kiwanja kingine, na inatokea anakamatwa huko nje na anakuwa anachafua taswira ya nchi” Amesema Rehema.

Pamoja na majadiliano mengone, Mamlaka na Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere wamekubaliana kushughulikia chngamoto zilizobainika zinazokwamisha juhudi za mapambano.

MWISHO.