Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA Yaeleza Mafanikio katika Vita Dhidi ya Biashara ya Dawa za Kulevya

Imewekwa: 01 July, 2019
 DCEA Yaeleza Mafanikio katika Vita Dhidi ya Biashara ya Dawa za Kulevya

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Tanzania imesema imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti uingizwaji wa dawa za kulevya huku ikieleza namna ambavyo wafanyabiashara wakubwa wa dawa hizo kufungwa na wengine kukimbia nchi.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Michuzi TV Kamishna wa Kinga na Tiba wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini Dk.Peter Mfisi amesema kwa sasa mamlaka imefanikiwa kudhibiti biashara ya dawa za kulevya.

Dk.Mfisi amefafanua hayo wakati Akifafanua zaidi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Dawa za Kulevya Duniani ambayo hufanyika kila ifikapo Juni 26 ya kila mwaka ambapo kwa Tanzania kitaifa yanafanyika katika Viwanja vya Tangamano jijini Tanga ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan.

" Katika kuhakikisha tunadhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini kwetu, Mamlaka yetu iliamua kuanza na kuwadhibiti wafanyabiashara wakubwa ambao wanajihusisha na biashara hii ikiwa pamoja na kuingiza nchini.

"Kulikuwa na wafanyabiashara waliokuwa anaingiza hadi kilo 100 za dawa za kulevya aina ya Heroin , baada ya kuwadhibiti hao kwa kuwakamata na kuwachukulia hatua ikiwa pamoja na kufungwa , tumefanikiwa kudhibiti biadhara hiyo.Pia kuna wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya ambao wamekimbia nchini yetu,"amesema Dk.Mfisi.

Pia amesema katika kukomesha biashara ya za kulevya wanatambua kuna wale wafanyabiashara wadogo wadogo lakini hawakuanza na hao kwani walijua kuna mahali ambapo wanazipata, hivyo walianza na wakubwa.

"Ripoti ya taasisi za kimataifa za kudhibiti biashara ya dawa za kulevya zinaonesha Tanzania imefanikiwa kupunguza uingizwaji wa dawa za kulevya kwa asilimia 90, hivyo imebaki asilimia 10 na ukweli tumefanikiwa sana,"amesema Dk.Mfisi.

Pamoja na mambo mengine Dk.Mfisi amezungumzia hatua ambazo zimechukuliwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupamba na Dawa za Kulevya katika kuhakikisha inadhibiti njia ambazo zilikuwa zinatumika kupitisha dawa za kulevya.

Amesema kuwa Mamlaka kwa sasa imekuwa makini kuhakikisha dawa za kulevya hazipiti kwenye mipaka ya nchi yetu kwa kuimatisha ulinzi ukiwemo kwenye Pwani ya Bahari ya Hindi ambayo ilikuwa inatumika sana huko nyuma.

"Tumefanikiwa kudhibiti Pwani ya Bahari ambako wafanyabiashara walikuwa wanatumia kama njia ya kupitisha dawa hizo.Hivyo wameamua kutumia Pwani ya Msumbiji na Afrika Kusini na kisha wanatumia njia barabara ili kuifikisha wanakotaka kuipeleka,"amesema Dk.Mfisi.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli iko makini katika kukabiliana na dawa za kulevya nchini na ukweli uliopo wote wanaojihusisha na biashara hiyo wamechukuliwa hatua stahiki.