Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

Elimu kwa Jamii: Nguzo Muhimu katika Kampeni za Kupinga Dawa za Kulevya

Imewekwa: 16 December, 2024
Elimu kwa Jamii: Nguzo Muhimu katika Kampeni za Kupinga Dawa za Kulevya

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeimarisha juhudi zake katika kupambana na usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya nchini kwa kupanua kampeni za elimu kwa umma na kufikia makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwa ni hatua muhimu katika kutekeleza nguzo ya kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya. Kwa kipindi cha mwezi mmoja, DCEA kupitia ofisi za kanda, imejizatiti kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, huku ikishirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa.

Kuanzia tarehe 10 hadi 13 Desemba 2024, DCEA Kanda ya Ziwa ilishiriki katika mafunzo maalum kwa maafisa kutoka vyombo vya ulinzi na usalama (Uhamiaji, Polisi, Mamlaka ya Bandari (TPA), na Uvuvi) jijini Mwanza. Mafunzo haya yalilenga kuihusisha jamii katika kupambana na uhalifu katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria. Yakiandaliwa na Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM), mafunzo haya yalitoa elimu kuhusu hatari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya, pamoja na namna ya kushirikisha jamii katika kukabiliana na tatizo hili.

Aidha, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini iliwanoa askari wanafunzi 759 katika Chuo cha Magereza Kiwila Songwe, ambapo walipatiwa mafunzo kuhusu kudhibiti usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya. Kanda ya Pwani ilifanya kampeni ya elimu kwa jamii kupitia kampeni ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, ikiwa ni pamoja na wawakilishi wa wanawake kutoka kata 18 na makundi mbalimbali ya wanawake wa mitaa ya Mtwara Mikindani, pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.

Vilevile, Kanda ya Kati, kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Mirembe na Asasi ya Vanessa Amada Foundation, ilitoa elimu kwa wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dodoma. Wanafunzi hao walielimishwa kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya na walihimizwa kutatua changamoto za kiuchumi, kijamii, na kitaaluma kwa njia bora na sahihi.

Kando na hayo, Kanda ya Kaskazini ilitoa elimu kwa skauti 230 katika Kambi ya Kisongo, Arusha, huku Kanda ya Pwani ikitoa elimu kwa wanachuo 1,115 katika Chuo cha Clinical Officer Training Centre (COTC) Mtwara. Elimu hiyo ilijumuisha madhara ya dawa za kulevya, na washiriki walihamasishwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya kwa Mamlaka kupitia namba ya bure 119.

Pia, DCEA Kanda Maalum Dar es Salaam ilishiriki katika Tamasha la BIBI TITI FESTIVAL lililofanyika Ikwiriri, Rufiji, Mkoa wa Pwani, ambapo elimu ilitolewa kupitia banda maalum. Mgeni rasmi katika tamasha hilo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Ndugu John Mongela, ambaye alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Pamoja na elimu kutolewa kwa makundi mbalimbali ya kijamii, DCEA ilishiriki katika Mkutano wa Mashauriano ya Umoja wa Afrika juu ya Kupunguza Uhitaji wa Dawa za Kulevya barani Afrika, uliofanyika Arusha kuanzia tarehe 10 hadi 13 Desemba 2024. Mkutano huu, uliohusisha zaidi ya nchi 30 wanachama wa Umoja wa Afrika, ulilenga kuimarisha juhudi za kutoa elimu sahihi kwa jamii na kupanua huduma za matibabu na utengamao kwa watu wanaokabiliwa na uraibu wa dawa za kulevya. DCEA ilishiriki kwa kubadilishana uzoefu na mikakati bora ya kukabiliana na matatizo ya dawa za kulevya.

Kwa jumla, DCEA inaendelea vema katika kupambana na dawa za kulevya nchini Tanzania kupitia mkakati wa kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya, ushirikiano wa kitaifa, kikanda na  kimataifa. Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, DCEA inaendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara ya dawa za kulevya na kutoa fursa za kushiriki katika mapambano dhidi ya janga hili.