Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA yashiriki Maonesho ya Sabasaba

Imewekwa: 08 July, 2024
DCEA yashiriki Maonesho ya Sabasaba

Mamlaka ya Kudhiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA inashiriki Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Katika Maonesho haya, Mamlaka ina mabanda mawili ambapo moja liko kwenye banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu na banda lingine lipo katika Banda la Katavi.

Katika mabanda hayo, elimu juu ya tatizo la dawa za kulevya hususani kuhusu mikakakati mikuu minne inayotumika katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya inatolewa kwa wananchi. Mamlaka inashiriki maonesho haya punde tu baada ya Kumaliza Maadhimisho ya Kitaifa ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya ambapo kitaifa yalifanyika jijini Mwanza huku yakichagizwa na kauli mbiu ‘‘Wekeza kwenye kinga na tiba dhidi ya dawa za kulevya’’.

Kwa mantiki hiyo, utoaji elimu unaoendelea katika viwanja vya sabasaba ni utekelezaji wa kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwani elimu inayotolewa kwa jamii inalenga kuikinga jamii isijiingize kwenye matumizi wala biashara ya dawa za kulevya kwa namna yoyote. Aidha, watu wanaoendelea kutembelea mabanda ya Mamlaka hufahamishwa aina za tiba kwa waraibu wa dawa za kuleya na upatikanaji wake.

Hivyo, Mamlaka ya Kudhiiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inawaalika wananchi wa Dar es Salaam na maeneo ya karibu kutumia fursa hii kutembelea mabanda ya Mamlaka ili kupata uelewa juu ya tatizo la dawa za kulevya.

Baadhi ya wananchi wameendelea kujifunza kuhusu dawa za kulevya na utendaji wa Mamlaka katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es salaam.

 

Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ametembelea Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo lipo Banda la Mamlaka katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba). Rais Kikwete ameipongeza Mamlaka kwa jitihada zinazofanyika katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Deogratius John Ndejembi akipata maelezo kutoka kwa Kamishna msaidizi wa Kinga na Huduma za Jamii Bi Moza Makumbuli wakati alipotembelea Banda la ofisi ya Waziri Mkuu katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba).

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka akipewa maelezo na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz wakati alipotembelea Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu katika banda la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya .

Wananchi mbalimbali mameendelea kutembelea Banda la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya lililopo katika banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupata elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya.