Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA YAKAMATA KILO 54,506 ZA DAWA ZA KULEVYA, WATUHUMIWA 72 MBARONI.

Imewekwa: 04 April, 2024
DCEA YAKAMATA KILO 54,506 ZA DAWA ZA KULEVYA, WATUHUMIWA 72 MBARONI.

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wakala wa misitu Tanzania (TFS) imefanya operesheni katika mikoa sita na kufanikiwa kukamata jumla ya kilo 54,506.553 za dawa za kulevya. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Kamishna Jenerali wa DCEA  Aretas Lyimo, amesema operesheni hiyo imefanyika katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Iringa, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam. Dawa zilizokamatwa ni bangi kilogramu 54,489.65, mirungi kilogramu 10.3, heroin gramu 90.93, cocaine gramu 1.98 na kilogramu 4.623 za aina mpya ya dawa ya kulevya inayoitwa methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) iliyokamatwa jijini Dar es Salaam ikisafirishwa na raia wa Comoro anayeitwa Ahmed Bakar Abdou (32).

Kamishna Lyimo amesema, Methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) ni dawa mpya ya kulevya iliyo katika kundi la vichangamshi inayotengenezwa kwa kutumia kemikali bashirifu.  ‘’Dawa hii ina kemikali inayoweza kuleta madhara ya haraka kwa mtumiaji ikilinganishwa na dawa nyingine za kulevya. Pia, imeongezwa nguvu ya kilevi inayozidi cocaine, heroin na methamphetamine,’’ amesema Lyimo.

Aidha, ameongeza kuwa,  dawa hiyo huuzwa kwa njia ya mtandao na husafirishwa kupitia kampuni za usafirishaji vifurushi na hufichwa kwa kuwekwa chapa za majina bandia kama vile bath salts, Ivory Wave, plant fertilizer, Vanilla Sky, na Energy. ameendelea kusema kuwa, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya imebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika hifadhi za misitu mkoani Shinyanga na Tabora ambapo wahalifu hao wamekata miti na kulima bangi. 

"Tumebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika hifadhi za misitu ya Ubangu mkoani Shinyanga na Mabatini mkoani Tabora ambapo wahalifu hao wamekata miti katikati ya misitu hiyo na kulima bangi. Kwa ushirikiano tulioupata kutoka kwa wakala wa misitu (TFS) tulifanikiwa kuteketeza mashamba hayo na kuwakamata wahusika" amesema Lyimo.

Pia amewashukuru wananchi kwa kutoa taarifa zilizopelekea kufanikisha ukamataji wa dawa za kulevya na ametoa wito kwa jamii kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya  katika kutokomeza matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini.

‘’Tunatoa shukrani zetu kwa wananchi kwa kutoa taarifa sahihi kuhusu wazalishaji na wauzaji wa dawa za kulevya katika maeneo yao na tutaendelea kushirikiana na wadau na jamii kwa ujumla ili kufanikisha operesheni zetu," amesema Lyimo.

Picha 1: Uteketezaji wa shamba la bagi katika misitu ya Ubangu mkoani Tabora.

Picha 2: Dawa ya kulevya inayoitwa methylene dioxy pyrovalerone (MDPV) iliyokamatwa jijini Dar es Salaam

Picha 3: Kamishna Jenerali Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uiofayika karika ofisi za DCEA jijini Dar es Salaam. 

Picha 4: Uteketezaji wa dawa za kulevya.

MWISHO