DCEA NA TPC WAINGIA MAKUBALIANO KUDHIBITI USAFIRISHAJI WA DAWA ZA KULEVYA KUPITIA MTANDAO WA POSTA
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) wametia saini Hati ya Ushirikiano, ikilenga kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kemikali bashirifu, na dawa tiba zenye asili ya kulevya kupitia mtandao wa posta. Makubaliano hayo yaliwekwa saini tarehe 19 Desemba, 2024 na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas James Lyimo, na Postamasta Mkuu wa TPC, Bw. Macrice Daniel Mbodo, ikielezwa kuwa hatua muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.
DCEA imebainisha kuwa wahalifu wamekuwa wakitumia mbinu za kusafirisha dawa za kulevya kupitia vifurushi na mizigo. Baadhi ya dawa zilizokamatwa ni mirungi (kilo 39,928.99), heroin (gramu 1,304.17), cocaine (gramu 673.55), pamoja na dawa za tiba zenye asili ya kulevya kama morphine na codeine. Ushirikiano huu utajumuisha mafunzo ya watumishi, kuboresha vifaa vya utambuzi, na kubadilishana taarifa kwa wakati ili kuimarisha ufanisi wa ukaguzi.
Aidha, Postamasta Mkuu Bw. Mbodo alisisitiza kwamba Shirika la Posta limejipanga kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa bidhaa kupitia mtandao wake na kusisitiza kuwa mtandao wa Posta hautaruhusu bidhaa haramu kama dawa za kulevya, silaha, na nyara za serikali kupita bila kugundulika.
“Teknolojia ya kisasa imerahisisha usafirishaji wa dawa mpya za kulevya kupitia mifumo ya kifedha ya kidijitali na majukwaa ya siri kama 'dark web.' Hata hivyo, mtambo wa kisasa uliotolewa na DCEA umeimarisha uwezo wa TPC kubaini dawa hizo bila kufungua vifurushi, hatua ambayo imekuwa nyenzo muhimu kwa kukabiliana na changamoto hizi,” alisisitiza Bw. Mbodo.
Kamishna Jenerali Lyimo alieleza kuwa ushirikiano huu unatoa ujumbe wa wazi kwa wahalifu kuwa vitendo vyao havitavumiliwa na aliwashukuru wadau wote wanaoshiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya.
Wanasheria kutoka DCEA na TPC wakiwaongoza viongozi wao kusaini Hati ya Makubaliano.
Kamishna Jenerali Aretas Lyimo akisaini Hati ya Ushirikiano kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kemikali bashirifu, na dawa tiba zenye asili ya kulevya kupitia mtandao wa posta.
Postamasta Mkuu wa TPC, Bw. Macrice Daniel Mbodo akisaini Hati ya Ushirikiano kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kemikali bashirifu, na dawa tiba zenye asili ya kulevya kupitia mtandao wa posta.
Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo akizungumza na wageni waliolikwa kushuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo.
Baadhi ya wageni walioudhuria tukio hilo katika makao makuu ya DCEA, Kivukoni, Dar es Salaam.
Postamasta Mkuu wa TPC, Bw. Macrice Daniel Mbodo akizungumza na wageni walioalikwa kushuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo.
xx MWISHO xx