Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya

( DCEA )

Kesi ya Abdul Nsembo na mkewe Shamimu Mwasha sasa kusikilizwa Mahakama Kuu

Imewekwa: 04 May, 2020
Kesi ya Abdul Nsembo na mkewe Shamimu Mwasha sasa kusikilizwa Mahakama Kuu

Shauri la uhujumu uchumi namba 36 la mwaka 2019 la kusafirisha dawa za kulevya linalomuhusisha mshtakiwa Abdul Issa Nsembo na mkewe Shamim Mwasha limehamishiwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa.

Washtakiwa wanakabiliwa na kosa la kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha sheria, ambapo walikamatwa tarehe 1 mwezi Mei 2019, eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam wakiwa na gramu 232.70 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Kesi dhidi yao ilisajiliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kama Shauri la Uhujumu uchumi la mwaka 2019. Shauri hilo liliendelea kutajwa katika mahakama hiyo hadi tarehe 30 mwezi Aprili 2020 ambapo washtakiwa walifanyiwa taratibu za kisheria za kuhamisha shauri kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwenda Mahakama Kuu, mbele ya Hakimu Mkazi Godfrey Isaya baada ya upelelezi kukamilika.

Shauri hilo tayari limehamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi kwa ajili ya hatua za usikilizwaji kadri itakavyopangwa na msajili wa Mahakama hiyo.

Katika maelezo yaliyosomwa mbele ya mahakama; upande wa Mashtaka ulidai kwamba mshtakiwa wa kwanza Abdul Nsembo anatuhumiwa kufadhili biashara ya dawa za kulevya kwa muda mrefu huku akiwa na mtandao mkubwa ndani na nje ya nchi.

Washtakiwa wote wawili wamerudishwa mahabusu kuendelea kusubiri taratibu kwani makosa wanayoshtakiwa nayo hayana dhamana.