Ni nini kinachosababisha mtu kutumia dawa za kulevya?
Matumizi ya dawa za kulevya yameendelea kuwa changamoto katika jamii yetu hasa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 14-24. Vijana wengi hujihusisha na matumizi hayo wakiwa katika shule za msingi na sekondari hivyo kuathiri makuzi yao kimwili na kiakili. Matumizi ya dawa za kulevya huchangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo za kifamilia, kijamii na kiuchumi. Miongoni mwa sababu hizo ni:
i. Msukumo rika na kufuata mikumbo, ambapo baadhi ya vijana hurubuniwa na kushawishiwa na wenzao wanaotumia dawa hizo. Tatizo hili huwapata mara nyingi vijana wenye malezi duni, wenye mazingira magumu na hatarishi ya kuishi kama vile migodini na watoto wa mitaani.
ii. Kushindwa kujitambua (stadi za maisha) miongoni mwa vijana. Hali hii huwasababishia kujiingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa sababu ya kukosa uwezo wa kutambua changamoto zao na njia sahihi za kutatua changamoto hizo.
iii. Migogoro na utengano wa kifamilia imekuwa ikisababisha kukosekana kwa malezi bora kwa watoto na vijana hali inayosababisha kukosekana kwa uangalizi wa karibu na hivyo baadhi yao kujiunga na makundi yanayotumia dawa za kulevya
iv. Urahisi na upatikanaji wa dawa za kulevya katika mazingira yetu kama vile bangi na mirungi imekuwa moja ya sababu kubwa ya watu kushawishika kuingia kwenye matumizi ya dawa hizo.
v. Kutokuwa na uelewa sahihi juu ya madhara yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya kiafya, kijamii na kiuchumi. Asilimia kubwa ya watu wanajiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya kwa lengo la kupata starehe, furaha, kuwa karibu na marafiki au kupunguza makali ya maisha bila kufahamu madhara wanayoweza kuyapata.
vi. Kurithi vinasaba vya uraibu, familia ambazo zimeathirika na uraibu na kuwa na vinasaba hivyo husababisha wanafamilia kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya. Wazazi wenye uraibu wa dawa za kulevya wana uwezekano mkubwa wa kupata mtoto wenye tatizo hilo.
vii. Watu wenye magonjwa ya akili kama vile saikosisi (kuchanganyikiwa), msongo wa mawazo, sonona na kihoro wamekuwa wakitumia dawa za kulevya kama njia ya kustahimili magonjwa hayo.
viii. Ukuaji wa teknolojia, utandawazi na mitandao ya kijamii vimechangia sana kwenye mmomonyoko wa maadili kwa vijana kwa kuiga maisha, mitindo, mila na desturi za kigeni ikiwemo kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya.
ix. Kuishi na ndugu, rafiki, mpenzi au mwenza ambaye anajihusisha na dawa za kulevya huchangia katika kuanza matumizi hayo.
x. Matumizi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya bila kufuata ushauri wa daktari. Mfano, mgonjwa akitumia dawa tiba zenye asili ya kulevya kutuliza maumivu anapoamua kutumia kinyume na utaratibu wa tiba alioandikiwa na Daktari, humsababishia kuwa mraibu wa dawa hizo.
xi. Imani potofu, mila na desturi za baadhi ya jamii zimekuwa zikichangia matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mfano, watu huamini wakitumia bangi hupata nguvu za kufanyakazi zaidi au kusoma zaidi.