Tanzania Yasisitiza Ushirikiano wa Kikanda Kupambana na dawa za Kulevya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu), Mheshimiwa Prof. Palamagamba A.J.M. Kabudi (Mb), amezitaka Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini kuimarisha ushirikiano na ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijensia kwa lengo la kubaini makundi ya wahalifu, kuvunja mitandao yao, pamoja na kuimarisha usalama na ulinzi wa mipaka.
Prof. Kabudi alitoa wito huo tarehe 15 Oktoba 2026, jijini Pretoria, Afrika Kusini, alipokuwa akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tatu wa Mawaziri wa Kituo cha Pamoja cha Mipango cha Nchi Tatu (Trilateral Planning Cell – TPC), utaratibu wa ushirikiano wa pande tatu unaozihusisha nchi hizo.
Mkutano huo ulijadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na biashara haramu ya dawa za kulevya katika ukanda wa Bahari ya Hindi, pamoja na aina nyingine za uhalifu wa kuvuka mipaka ya nchi, ikiwemo usafirishaji haramu wa binadamu na utekaji nyara. Washiriki pia walijadili changamoto zinazotokana na wahalifu kutumia mianya ya kiusalama katika mipaka na udhaifu wa mifumo ya kitaasisi kuwezesha vitendo vya uhalifu. Katika hatua nyingine, Mawaziri waliidhinisha maombi ya Angola na Uganda ya kujiunga na TPC, hatua inayoongeza idadi ya wanachama wa utaratibu huo kufikia nchi tano ambazo ni Angola, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania na Uganda. Makao makuu ya TPC yako nchini Msumbiji.
Akizungumza katika hotuba yake ya kufunga mkutano huo, Prof. Kabudi aliwakaribisha washiriki wa TPC nchini Tanzania, ambayo inatarajiwa kuwa mwenyeji mwenza wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ya mwaka 2027, kwa kushirikiana na Kenya na Uganda. Alihimiza nchi wanachama wa TPC kutumia mashindano hayo kama fursa ya kuendeleza juhudi za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu unaohusiana nayo, akibainisha kuwa matukio makubwa ya kimataifa ya michezo yanaweza pia kutumiwa na mitandao ya wahalifu kuwezesha shughuli haramu.
Mikutano ya TPC inalenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama katika kukabiliana na biashara haramu ya dawa za kulevya na aina nyingine za uhalifu wa kuvuka mipaka ya nchi.
DCEA YASHIRIKI MKUTANO WA MAOFISA WAKUU WA TPC
Kabla ya Mkutano wa Mawaziri, tarehe 14 Oktoba 2026, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas J. Lyimo, aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Maofisa Wakuu wa TPC. Mkutano huo uliwakutanisha maofisa na wataalamu wa kiufundi kutoka taasisi zinazohusika na udhibiti wa dawa za kulevya katika nchi zinazoshiriki, kwa lengo la kujadili uhalifu unaohusiana na dawa za kulevya, kubadilishana uzoefu wa kiutendaji na kubaini suluhisho la changamoto zinazoathiri juhudi za kudhibiti dawa za kulevya.
Mkutano wa Maofisa Wakuu ulifanyika kabla ya Mkutano wa Mawaziri na kuandaa mapendekezo ya kuimarisha ushirikiano kupitia TPC, kwa ajili ya kujadiliwa na Mawaziri. Mikutano hiyo pia ilihudhuriwa na maofisa waandamizi kutoka mamlaka za udhibiti wa dawa za kulevya, vyombo vya sheria na washirika wa maendeleo, wakiwemo Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Umoja wa Ulaya, pamoja na wawakilishi kutoka Comoro, Shelisheli, Eswatini, Uingereza na Marekani.
UNODC imetoa ufadhili na msaada wa uratibu kwa shughuli za TPC, ikiwemo maandalizi ya mikutano hiyo.

_1792251857.jpg)
hhhhh






