Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA YADHIBITI MTANDAO WA KIMATAIFA WA DAWA ZA KULEVYA, WATUHUMIWA SABA WAKAMATWA TANZANIA NA KENYA

Imewekwa: 09 November, 2026
DCEA YADHIBITI MTANDAO WA KIMATAIFA WA DAWA ZA KULEVYA, WATUHUMIWA SABA WAKAMATWA TANZANIA NA KENYA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB), imefanikiwa kudhibiti mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya baada ya operesheni zilizofanyika Tanzania na Kenya na kufanikisha ukamataji wa paketi 753 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine pamoja na watuhumiwa saba.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Novemba 9, 2026, Kamishna Jenerali Lyimo amesema operesheni hizo zilifanyika tarehe 6 na 7 Novemba 2026 katika eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam, na Kwale, Mombasa nchini Kenya, kwa kushirikiana na Kitengo cha Kitaifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB).

Katika operesheni ya kwanza iliyofanyika tarehe 6 Novemba 2026, eneo la Mwenge, jijini Dar es Salaam, DCEA ilikamata paketi 299 za dawa za kulevya, zikiwemo paketi 24 za heroin na paketi 275 za methamphetamine. Dawa hizo zilikuwa zimefichwa ndani ya magari mawili aina ya Ford Ranger yenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ, ambayo pia yanashikiliwa kutokana na kuhusishwa na uhalifu huo.

Katika operesheni hiyo, watuhumiwa wanne walikamatwa. Watuhumiwa hao ni JUMA SLAATI KISOMEKO (36), raia wa Uganda, dereva na mkazi wa Piji, nchini Uganda; ISSA SAID NASSORO (34), mfanyabiashara; IBRAHIM SAID CHEMBELA (30), dereva; na MOHAMED ALLY SHEMTUU (45), dereva. Watuhumiwa watatu wa mwisho ni wakazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamishna Jenerali Lyimo, baada ya kukamatwa na kuhojiwa, watuhumiwa hao walieleza kuwa dawa hizo walizichukua Mombasa, nchini Kenya, na kuzisafirisha kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro, mkoani Tanga. Kutokana na maelezo hayo, DCEA iliwasiliana na mamlaka husika nchini Kenya na kushirikiana kiutendaji ili kubaini chanzo cha dawa hizo, eneo lililotumika kuzihifadhi pamoja na kuwabaini wahusika wengine wa mtandao huo.

Kupitia ushirikiano huo, tarehe 7 Novemba 2026, DCEA kwa kushirikiana na NANB ilifanikiwa kukamata paketi nyingine 454 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine katika operesheni iliyofanyika eneo la Kwale, Mombasa nchini Kenya.

Katika operesheni hiyo, watuhumiwa wengine watatu walikamatwa. Watuhumiwa hao ni SALEH KHAMIS BASELEMAN (45), maarufu kama MBWIGA, raia wa Tanzania, mfanyabiashara na mkazi wa Mombasa, nchini Kenya; SEIF SAID HAMAD (54), maarufu kama BABU SEIF, raia wa Tanzania, mvuvi na mkazi wa Kinondo, Mombasa, nchini Kenya; na ZURAICAH AHMED HUSSEIN (25), raia wa Uganda, mfanyabiashara na mkazi wa Shirazi, Mombasa, nchini Kenya.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa ni vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya ambao unafanya shughuli zake katika nchi mbalimbali, zikiwemo Afghanistan, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Tanzania na Dubai.

Ameeleza kuwa mmoja wa watuhumiwa hao, SALEH KHAMIS BASELEMAN, maarufu kama MBWIGA, anadaiwa kununua dawa za kulevya moja kwa moja kutoka Afghanistan na kuzisafirisha kwa njia ya bahari hadi katika fukwe za Mombasa, nchini Kenya, kabla ya kuzisambaza katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.

Aidha, mtuhumiwa huyo anahusishwa na ukamataji wa tani 3.5 za dawa za kulevya uliofanywa na DCEA mwezi Desemba 2023 katika eneo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam, na mkoani Iringa.

Kwa sasa, taratibu za kisheria kati ya Tanzania na Kenya zinaendelea ili kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema mafanikio yaliyopatikana katika operesheni hizo yanaonesha umuhimu wa ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.

Aidha, DCEA inatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uwepo wa biashara na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwezesha hatua za haraka za kudhibiti na kupambana na uhalifu huo.