Tanzania Yaimarisha Ushiriikiano wa Kimataifa Katika Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amefanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Vienna (UNOV) na Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Dkt. Monica Juma, katika hatua ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na UNODC katika juhudi za kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Mazungumzo hayo yamefanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 70 wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), unaoendelea jijini Vienna, Austria, ambapo Tanzania imeshiriki katika shughuli mbalimbali za kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, pande hizo zimejadili umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto zinazohusiana na dawa za kulevya, hususan katika kipindi ambacho tatizo hilo linabadilika kwa kasi na kuhitaji mikakati inayozingatia mazingira na changamoto za sasa.
Ushirikiano kati ya Tanzania na UNODC ni sehemu muhimu ya juhudi za nchi katika kuimarisha hatua za kinga, udhibiti, utekelezaji wa sheria na upatikanaji wa mbinu bora za kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya.
Mazungumzo hayo yamefanyika wakati Tanzania ikiendelea kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kikanda na kimataifa yanayolenga kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu za kisasa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Katika muktadha huo, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Vienna, Austria, Bi. Naimi Azizi, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, pamoja na ujumbe wa Tanzania, walishiriki katika Mkutano wa 33 wa Vyombo vya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa Nchi za Afrika, uliofanyika tarehe 8 hadi 11 Septemba 2026 jijini Vienna, Austria.
Mkutano huo ulijadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya barani Afrika, ikiwemo matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, pamoja na kubadilishana uzoefu na taarifa kuhusu mwenendo wa tatizo la dawa za kulevya.
Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo umeendelea kutoa fursa kwa nchi kujifunza uzoefu na mbinu zinazotumika katika mataifa mbalimbali, kujenga na kuimarisha mitandao ya ushirikiano, pamoja na kupata maarifa yanayoweza kusaidia kuboresha mikakati ya kitaifa ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Kwa kushiriki katika majadiliano ya kikanda na kimataifa pamoja na kuimarisha ushirikiano na UNODC, Tanzania inaendelea kusisitiza umuhimu wa hatua za pamoja katika kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya, likizingatia mabadiliko ya mwenendo wa tatizo hilo na matumizi ya teknolojia katika uhalifu unaohusiana na dawa za kulevya.
Mazungumzo hayo ya Makamu wa Rais na uongozi wa UNODC, pamoja na ushiriki wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa ya kudhibiti dawa za kulevya, yanaakisi dhamira ya nchi ya kuendeleza ushirikiano wa kimataifa na kutumia maarifa, uzoefu na mbinu za kisasa katika kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.





