Kilo 18,078 Za Dawa Za Kulevya Zakamatwa Katika Operesheni Za Mikoa 14
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema Mamlaka imekamata jumla ya kilogramu 18,078.41 za dawa za kulevya katika operesheni zilizofanyika katika mikoa 14 nchini katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu operesheni na hatua zilizochukuliwa na Mamlaka katika kipindi hicho, Lyimo amesema ukamataji huo umehusisha kilogramu 11,504.76 za bangi, kilogramu 6,529.5 za mirungi, kilogramu 44.45 za bangi aina ya skanka na gramu 41.25 za heroin.
Operesheni hizo zilifanyika katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Dodoma, Mbeya, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Katika operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 289 walikamatwa, ambapo 169 wamefikishwa mahakamani, huku taratibu za kisheria zikiendelea dhidi ya watuhumiwa wengine.
Matokeo ya operesheni hizo yanaonesha kuwa bangi imeendelea kuongoza kwa kiwango cha uzalishaji na ukamataji, hususan katika mikoa ya Morogoro na Tabora. Mkoani Morogoro, DCEA ilikamata kilogramu 6,299.24 za bangi pamoja na kilogramu 226 za mbegu za bangi, huku mkoani Tabora kilogramu 4,650.86 za bangi pamoja na kilogramu 203 za mbegu za bangi zilikamatwa.
Kwa upande wa mirungi, Lyimo amesema operesheni zimebaini matumizi ya pikipiki, mabasi na magari ya abiria katika usafirishaji wa dawa hiyo, hususan katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Dodoma, ambapo jumla ya kilogramu 6,412.89 za mirungi zilikamatwa.
Katika moja ya matukio hayo, watuhumiwa watatu walikamatwa wakisafirisha bunda 238 za mirungi zenye uzito wa kilogramu 125.33 kwa kutumia basi la kampuni ya RATCO, lenye namba za usajili T.443 EMG, lililokuwa likifanya safari kati ya Tanga na Dar es Salaam.
Aidha, mkoani Tabora, Wilaya ya Uyui, kilogramu 21.95 za bangi zilikamatwa katika gari aina ya TATA lenye namba za usajili T.381 DWU, lililokuwa likifanya safari kati ya Uyui mkoani Tabora na Kahama.
DCEA yaimarisha udhibiti wa vyombo vya usafiri
Lyimo amesema operesheni hizo zimewezesha pia kukamatwa kwa pikipiki 40, bajaji moja na magari nane yaliyohusishwa na tuhuma za usafirishaji wa dawa za kulevya. Miongoni mwa magari yaliyokamatwa ni Toyota Harrier yenye namba T.878 ASJ, Toyota Land Cruiser T.234 BUR, Toyota IST T.215 DCJ, Toyota Noah T.231 AWP, Toyota Alphard T.870 EDE pamoja na Toyota Discovery. Kutokana na hali hiyo, DCEA imewataka wamiliki na waendeshaji wa mabasi na magari ya abiria kuimarisha udhibiti wa mizigo, ukaguzi wa vyombo vya usafiri na usimamizi wa wafanyakazi ili kuzuia vyombo vyao kutumika katika usafirishaji wa dawa za kulevya.
Katika eneo la ukaguzi wa abiria katika Bandari ya Dar es Salaam, Mamlaka pia ilibaini matukio ya usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia abiria. Mbali na Watanzania waliokamatwa, DCEA ilimkamata raia wa Uturuki akiwa na gramu 1.87 za bangi aina ya skanka, raia wa Kenya akiwa na gramu 3.89 za mirungi na raia wa Nigeria akiwa na gramu 4.6 za bangi. Aidha, katika operesheni zilizofanyika mkoani Arusha, raia wawili wa Afrika Kusini walikamatwa wakiwa na jumla ya gramu 65.8 za bangi aina ya skanka.
DCEA yazuia shehena ya kemikali, yaonya dhidi ya rushwa
Katika eneo la udhibiti wa kemikali, Lyimo amesema DCEA, kupitia uchambuzi wa mfumo wa kielektroniki, ilizuia kuingia nchini kwa shehena ya sulphuric acid yenye uzito wa kilogramu milioni 64 baada ya kubaini kuwa taarifa zilizowasilishwa kuhusu uingizaji wa kemikali hiyo hazikuwa sahihi na matumizi yake halali hayakuwa yamebainishwa.
Pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Kamishna Jenerali amesema Mamlaka imebaini kuwepo kwa baadhi ya watendaji wasio waaminifu walio nje ya Mamlaka wanaodaiwa kutumia mwanya katika udhibiti wa biashara ya dawa za kulevya kujihusisha na vitendo vya rushwa na uhalifu. Amesema baadhi ya watu hao wamekuwa wakiwalenga wahalifu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, kuwakamata na kuwanyang’anya dawa hizo, kisha kuwashinikiza kutoa rushwa. Katika baadhi ya matukio, wamekuwa wakiwatishia kuwafikisha katika Mamlaka endapo watakataa kutekeleza matakwa yao.
DCEA imetoa onyo dhidi ya vitendo hivyo na kuwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na dawa za kulevya kwa namna yoyote ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Kamishna Jenerali amesema ushirikiano wa wananchi, wamiliki na waendeshaji wa vyombo vya usafiri pamoja na wadau wengine ni muhimu katika kuimarisha udhibiti na kuzuia matumizi ya njia mbalimbali katika usafirishaji wa dawa za kulevya.