Watuhumiwa wa Tani 1.8 za Skanka Wapandishwa Kizimbani
Watuhumiwa watano waliokamatwa kuhusiana na usafirishaji wa bangi aina ya skanka kiasi cha tani 1.8 wamefikishwa mahakamani jana tarehe 10 Septemba, 2024, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Washtakiwa hao ni Richard Mwanri (47) mkazi wa Mbezi Makonde na mama yake Felista Mwanri (70) mkazi wa Luguruni jijii Dar es Salaam. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Athuman Mohamed maarufu kama Makame (58) mkazi wa Tanga, Juma Chappa (36) mkazi wa Kiwalani, na Omary Mohamed (32) ambaye ni dereva na mkazi wa Buza, Dar es Salaam.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini Wakili wa Serikali, Eric Davis, alidai kuwa, washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kusafirisha aina hiyo ya dawa za kulevya kinyume na sheria. Alisema kuwa, mnamo Agosti 28, 2024, wakiwa eneo la Tairo Luguruni barabara ya Kwembe ndani ya Wilaya ya Ubungo, washtakiwa walikamatwa wakiwa na bangi yenye uzito wa kilogramu 1,815. Wakili Davis alifafanua kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa shauri hilo.
Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa kuwa kesi yao ni ya Uhujumu Uchumi, na kwa hivyo hawatapaswa kujibu chochote kwa sasa kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za aina hiyo na aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24, 2024 kwa ajili ya kutajwa na kupokea taarifa kuhusu maendeleo ya upelelezi.
MWISHO