DCEA Yazindua Vilabu vya Kupinga Dawa za Kulevya Vyuo Vikuu
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) imezindua rasmi Vilabu vya Kupiga Vita Dawa za Kulevya katika vyuo vikuu nchini, hatua inayolenga kuimarisha kinga dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na kuwashirikisha wanafunzi katika juhudi za kitaifa za kukabiliana na tatizo hilo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema Vilabu vya Kupiga Vita Dawa za Kulevya vitakuwa majukwaa muhimu ya kuwawezesha wanafunzi kupata na kusambaza elimu sahihi kuhusu dawa za kulevya, kuhamasisha maisha yasiyo na dawa za kulevya na kushiriki katika kutafuta majibu ya changamoto hiyo.
Amesema tatizo la dawa za kulevya lina athari kubwa kwa afya ya jamii, usalama, uchumi, familia na maendeleo ya Taifa, hivyo Serikali imeendelea kutekeleza mikakati inayolenga kupunguza upatikanaji wa dawa za kulevya, kupunguza uhitaji wake, kupunguza madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa, kikanda na kimataifa. Hivyo, uzinduzi wa vilabu hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kupunguza uhitaji wa dawa za kulevya, unaosisitiza kinga kupitia elimu, uhamasishaji na hatua zinazolenga kuwazuia watu kuanza kutumia dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali amesema wanafunzi wa vyuo vikuu ni kundi muhimu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutokana na nafasi yao katika kujenga mustakabali wa Taifa kwani ni vituo vya kuzalisha wataalamu, viongozi na maarifa yanayohitajika katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii, hivyo ushiriki wa wasomi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya una umuhimu mkubwa kwa Taifa.
“Tunahitaji taaluma na maarifa ya wasomi katika kusaidia Serikali kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya na kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi wa kisayansi na kitaaluma,” amesema Kamishna Jenerali.
Amehimiza wanafunzi, wahadhiri na wataalamu wa vyuo kujikita katika tafiti kuhusu sababu na vihatarishi vya matumizi ya dawa za kulevya, mwenendo wa tatizo, madhara yake pamoja na ufanisi wa hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana nalo. Ameongeza kuwa, kuna umuhimu wa kutumia taaluma mbalimbali katika kutafuta suluhisho la tatizo hilo, ambapo wataalamu wa afya wanaweza kuchangia tafiti kuhusu madhara ya kiafya na matibabu, wataalamu wa saikolojia na jamii kuchunguza sababu zinazochochea matumizi ya dawa za kulevya, wataalamu wa sheria kuchambua changamoto za utekelezaji wa sheria, huku wataalamu wa TEHAMA kusaidia kukabiliana na uingiaji, uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Kamishna wa Katiba, Sheria na Utawala Bora wa TAHLISO, Aroni Seni amesema kuanzishwa kwa vilabu hivyo kumetokana na kutambua athari zinazotokana na matumizi ya dawa za kulevya kwa vijana na nguvu kazi ya Taifa, hususan wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu.
“Vijana si watazamaji katika vita hivi, bali ni sehemu muhimu ya suluhisho. Kupitia klabu hizi tunataka kuwapa wanafunzi nafasi ya kushiriki katika elimu ya kinga, uhamasishaji na kujenga mazingira salama ndani ya taasisi zetu za elimu ya juu,” amesema.
Amebainisha kuwa pamoja na vyuo na vyuo vikuu kuwa vituo vya kuzalisha maarifa na wataalamu wa fani mbalimbali, mazingira ya vyuo yanaweza pia kuwa na vishawishi vinavyowaweka baadhi ya vijana katika hatari ya kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya. Vilabu hivyo vinatarajiwa kuwasaidia wanafunzi kuelimishana, kuhamasisha maisha yasiyo na dawa za kulevya, kuchochea mijadala ya kitaaluma, kuibua maeneo yanayohitaji utafiti na kuongeza ushiriki wa wanafunzi katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.