Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Waziri Mkuu

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya

( DCEA )

DCEA yakamata Tani 1.8 za skanka jijini Dar es Salaam

Imewekwa: 11 September, 2024
DCEA yakamata Tani 1.8 za skanka jijini Dar es Salaam

MAMLAKA  ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania (DCEA) imefanikiwa kumkamata Richard Henry Mwanri anayetuhumiwa kupokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali duniani na kuziingiza nchini kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine.

Mbali na hilo lakini pia imemkamata Felista Henry Mwanri (70) mkazi wa Luguluni Mbezi Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa za kulevya  zenye uzito wa tani 1.8 aina ya skanka

Hata hivyo DCEA imewaonya wamiliki wa nyumba nchini kuacha kujihusiasha na biashara za dawa za kulevya ikiwemo kuzihifadhi ndani ya nyumba zao na kushirikiana na wafanyabishara wa dawa hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Septemba 10,2024 Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) Aretas Lyimo amesema Agosti 28, 2024 hadi Septemba 2, 2024 Mamlaka ilifanya oparesheni katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni mkoani Dar es Salaam na kufanikiwa  kuwakamata watuhumiwa watano kuhusiana na biashara hiyo wakiwa na tani 1.8 za dawa za kulevya aina skanka.

Kamishna Lyimo amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Felista Henry Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguruni Mbezi Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya.

Watuhumiwa wengine  ni Athumani Koja Mohamed (58) mfanyabiashara, na mkazi wa Tanga, Omary Chande Mohamed (32) ambaye ni dereva bajaji na mkazi wa Buza mkoani Dar es Salaam, Juma Abdallah Chapa (36) mkazi wa Kiwalani mkoani Dar es Salaam.

Aidha Katika operesheni hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa.

‘’Richard Mwanri ni mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kusambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini.

‘’Kwa siku za hivi karibuni, dawa za kulevya aina ya skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara nchini ambapo Skanka ni aina ya bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, figo, na ini.

‘’Matumizi ya skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara kwa mtoto aliye tumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo’’ameeleza Kamishna Lyimo

Kamisha Lyimo amewasihi wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara hii haramu na kuhamasishana kutoshiriki katika biashara wala matumizi ya dawa za kulevya.

‘’Aidha, watumishi wanaofanya kazi katika vituo vya forodha vya mipakani hususani wanaohusika na ukaguzi wa magari na bidhaa zinazoingia na kutoka nchini, waendelee kuwa makini wanapotekeleza majukumu yao kwani wahalifu wa dawa za kulevya hubuni mbinu za kuficha ili kusafirisha dawa za kulevya.

‘’Ukamataji mkubwa wa dawa za kulevya unaofanyika nchini ni matokeo chanya ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali ya awamu ya sita, chini ya uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amedhihirisha dhamira ya kulinda kizazi cha sasa na kijacho kwa kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.

’Pia, ni matunda ya elimu ya dawa za kulevya inayoendelea kutolewa nchini ambayo imehamasisha wananchi kuwa na mwamko wa kutoa taarifa dhidi ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya’’ameongeza Kamishna Lyimo

DCEA itaendelea kuwa macho na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wote wanaoharibu nguvu kazi ya taifa kwa kujihusisha na dawa za kulevya kwa namna yoyote ile.

 Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.

Vifurushi vilivyokamatwa Luguruni mbezi ndani yake kukiwa na pakiti zenye dawa za kulevya aina ya bangi (skanka).

Muonekano wa pakiti za dawa za kulevya ndani ya vifurushi vilivyokamatwa Luguruni Mbezi Jijini Dar es Salaam.

Pakiti za dawa za kulevya aina ya bangi (skanka) baada ya kutolewa kwenye vifurushi.

Dawa za kulevya aina ya bangi (skanka) zilizokamatwa katika muonekano wa karibu.

 

MWISHO